Shuhuda

Mwalimu Christopher Mwakasege ametoa ushuhuda huo katika semina inayoendelea sasa katika viwanja vya Furahisha jijini Mwanza Semina hiyo yenye somo linaloitwa namna ambavyo Roho Mtakatifu awezavyo kukusaidia ili upokee kile unachokiomba imeanza tar 19-07-2011 na inatazamiwa kuisha tar 23-07-2011.


Alisema Roho mtakatifu akwambiavyo omba hiyo haina MJADALA ni kuingia kwenye maombi mpaka upate unachokiomba kwa kuwa gharama ya kuingia kwenye maombi ili kupata ulichotakiwa kukipata ni ndogo kuliko gharama ya kukosa kile ulichoambiwa ukipate katika Maombi hayo.

Roho mtakatifu anapokupa mzigo wa kuombea jambo anakupa na muda ukizembea muda huo ukipita kinakuwa ni kiporo, na kiporo kinaweza kikalika na kipo ambacho hakiliki. .

“Tulipoenda Israel na Fanuel Sedekia kisha akaanza kuumwa madaktari waliniambia ubongo wake kwa asilimia tisini haufanyi kazi. Lakini walishangaa kwa nini kila mara niko pale Hospitali wakasema kwa nini usikae tu Hotelini kisha ukawa unapiga simu kuulizia hali ya Mgonjwa? Wao hawakujua kwa nini naenda pale kwa kuwa suala la kupiga simu tu sio tatizo ningeweza kurudi Arusha kisha nikawa napiga simu.

Suala hapa ni kuwa nilikuwa naenda kila mara kwa ajili ya kumfanyia maombi, nilikuwa nakaa kandokando ya Bahari ya Galilaya nafanya maombi juu ya Sedikia kwa masaa sita nikitoka hapo nasikia upako wa ajabu sana kIsha napanda Taxi kuelekea Hospitali. Nikifika Hospitali madactari na watu wa ICU walikuwa washanifahamu hivyo naenda moja kwa moja kwenye chumba cha nguo nabadili nguo kIsha naingia ICU alikolazwa.

Nikifika nambana Mungu kwa maswali Mengi namuuliza Sedekia, hivi unaongea nini na Yesu muda wote huo si urudi? na kisha namuuliza Yesu, hivi Yesu si unafahamu kuwa Sedekia anamke ukimchukua mkewe atamuachia nani? Kisha baada ya maneno hayo naweka mkono juu yake. Nilipokuwa nikiweka mkono juu yake ghafla upako wote unakuwa kama umenyonywa.

Baada ya hapo narudi hotelini naanza tena kumuuliza Mungu hivi Mungu kama basi husikii maombi yangu sikia maombi ya watanzania kwa kuwa saa hiyo nilijua watanzania wengi wanamuombea Sedekia.

Inafikia wakati nakata tamaa lakini ndani yangu najisemea Mwakasege haiwezekani jitie moyo kisha nabadili aina ya maombi, kwa kuwa nilikuwa na nguo zake pamoja na passport yake nikawa naviweka kati kisha nikawa naanza maombi ya Yeriko, nikawa niko hotelini usiku nazunguka nguo zake na paspot yake huku nikifanya maombi.

Taratibu Mungu akaanza kuniambia kuwa sedekia harudi, Kipidi hicho mimi na familia yangu tulikuwa tumepanga kwenda kupumzika nchini Uingereza wakati wa skukuu ya Chrismass, na booking mpaka ya Hotel tulikuwa tumeshafanya, na watoto wote wako nyumbani wakijiuliza tunaendaje kupumzika wakati Sedekia anaumwa? Chrismass ikapita na mwaka mpya pia kisha Sedekia akafariki.

Baada ya kifo hicho sikuchoka nkarudi tena kwa Mungu nikamuuliza kwa nini Mungu umeamua kumchukua Sedekia mikononi mwangu? Mungu alinijibu vitu ambavyo siwezi kuvisema hapa.

Kila siku mimi ni mgeni katika maombi namhitaji ROHO anifundishe kwa upya kwa kuwa sijui vita gani ninakwenda kupambana nayo, Mungu anabaki kuwa Mungu kwa kuwa hufanya atakavyo





"Kila aliye na Mwana anao huo ushuhuda"
kwa hiyo kama una ushuhuda wowote ambao Mungu amekutendea usisite kututumia ili tuweze kuuchapisha uwasaidie na kuwajenga wengine kwa ajili ya utukufu wa Mungu.
Shuhuda za Matendo makuu ya Mungu zinaandaliwa kwa ajili ya kuchapishwa mahali hapa
Zifuatazo ni Shuhuda mbalimbali zilizochpishwa mahali hapa:

Nimepona Tumbo La Uzazi

Shukurani Ya Pekee

Kitabu Cha Damu Ya Yesu Kimenisaidia

Nina Nena Kwa Lugha

Nilisumbuliwa na Mgongo miaka 10

Mdogo wangu Amepona Macho kupitia DVD ya mzaliwa wa Kwanza

Nimepona Kupitia Majarida Ya Mana

Nimepona Kifua

Nimepona Tumbo La Uzazi


"Tangazeni wokovu wake siku kwa siku (kila siku hubirini) habari za utukufu wake  habari za maajabu yake"
(Zaburi 96:2,3)
Tunakukaribisha katika ukurasa huu muhimu ambao tutakuwa tunakuwekea habari za matendo ambayo Mungu anawatendea watu kupitia huduma mbalimbali alizotupa.
Kwa wakati huu Mungu ametupa kuwahudumia watu sehemu mbalimbali kwa njia ya mahubiri/mafundisho; kwa njia ya maombi; kwa njia ya mtandao; kwa njia ya simu; kwa njia ya majarida na vitabu; na kwa njia ya barua.
Tumeona na kuelezwa mambo mengi sana ambayo Yesu amekuwa akiyafanya kupitia huduma alizotupa.
Faida zake:
Si watu wengi wanaopenda kuwaeleza wengine mambo ambayo Mungu amewatendea. Lazima wana sababu zao mbalimbali zinazowafanya wasiseme habari hizo kwa uwazi. Lakini tunataka kukueleza ya kuwa kuna faida nyingi zinazopatikana kwa kushuhudia wengine mambo ambayo unajua Mungu anafanya kwako na kwa wengine. Kwa mfano tafakari faida zifuatazo za kushuhudia matendo makuu ya Mungu:

1. Kuthibitisha ya kuwa Yesu Kristo yuko hai na ya kuwa ndiye Mwana wa Mungu. Soma katika Matendo 3:1-16. Pia angalia Yohana 20:30,31 pale inaposema:

"Na kuna ishara nyingine nyingi alizozifanya Yesu mbele ya wanafunzi wake zisizoandikwa katika kitabu hiki. Lakini hizi zimeandikwa; ili mpate kuamini ya kwamba Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu; na kwa kuamini mwe na uzima kwa jina lake"

2. Kuwavuta watu na kuwaweka katika hali ya kuhubiriwa injili.
Yesu Kristo alisema, " Nami nikiinuliwa juu ya nchi, nitawavuta wote kwangu" ( Yohana 12: 32). Unapotangaza mambo ambayo Yesu anafanya sasa ni njia mojawapo ya kumwinua. Ukisoma katika Yohana 6:2 utaona imeandikwa hivi: " Na mkutano mkuu wakamfuata, kwa sababu waliziona ishara alizowafanyia wagonjwa"

Kuna wakati mmoja karibu miaka kumi hivi imekwisha kupita tuliletewa nguo nyumbani kwetu Arusha ya kijana wa kutoka Likamba aliyekuwa mgonjwa ili tuiombee. Huyo kijana alikuwa na uvimbe katika paji la uso wake ambalo hata baada ya kulazwa kwa matibabu hopitalini hakupona.

Tuliombea hiyo nguo, na akapelekewa. Hiyo nguo ilipomgusa tu usoni, uvimbe ule uliyeyuka na kupotea. Akapokea uponyaji wake toka kwa Yesu! Jambo hili lilifanya mama yake na ndugu zake watake kujua zaidi habari za nguvu zinazoponya namna hiyo. Walipoletwa kwetu tukawaeleza habari za Yesu na wakakubali kuokoka - tukawaongoza sala ya toba - wakaokoka. Hata sasa miaka kumi baadaye, bado wanaendelea na Yesu!

Jirani zao wengine ambao walikuwa wameoana lakini bila kujaliwa mtoto kwa miaka mitano walipata habari za Yesu anayejibu! Walipoletwa kwetu kuulizia habari hizi tukawaeleza habari za Yesu, wakakubali kuokoka - tukaomba nao wakaokoka! Tuliomba pia juu ya hitaji lao la mtoto - na Mungu akajibu na kabla ya mwaka mmoja kwisha toka wakati huo wakajaliwa kupata mtoto wa kiume!

Kwa sababu ya miujiza hii mfululizo, tukaitwa kijijini kwao kuhubiri injili na kuombea wenye shida. Tulikwenda kijijini hapo tukahubiri habari za Yesu, watu wengi wakaokoka na kupona magonjwa yao. Kumbuka mambo yote haya yalianza baada ya kijana mmoja kutangaza habari za uponyaji wake, ambao ndio uliowavuta wengine kuulizia habari za Yesu aliyemponya!

3. Kuwatia moyo waliokata tamaa na walio na mahitaji wajue ya kuwa Mungu anaweza kuwasaidia na wao pia katika matatizo yao.

Ni kwa njia hii hata Naamani alipata kupokea uponyaji wa ukoma uliokuwa unamsumbua. Ukisoma kitabu cha pili cha Wafalme 5:1-14 Naamani alipata habari za Mungu anayeponya kwa njia ya maelekezo ya watumishi wake kutoka kwa mwanamke kutoka nchi ya Israeli aliyekuwa anamhudumia mke wake.

Hata leo kuna watu wengi wanaoteseka katika matatizo yao kwa sababu tu hawajawahi kusikia habari za Yesu anayejibu maombi na kuponya magonjwa siku hizi.
Kuna wakati tulipigiwa simu kutoka Mbeya na mtu ambaye alikuwa amesikia habari za Yesu anayejifunua katika maisha yetu. Alisema ya kuwa anaumwa na anahitaji maombi - tukaomba pamoja naye kwenye simu, na Mungu akamponya wakati huo huo! Mwingine akatupigia simu kutoka Tukuyu - Mbeya akisema anaumwa na anaona hatapona alikuwa anahitaji tumuombee aokoke. Tukaomba naye kwenye simu - naye akaokoka!

Hawa walitupigia simu kwa kuwa walikuwa wameambiwa habari za Yesu tuliye naye - na walipowasiliana nasi tukawaelekeza kwa Yesu naye akawasaidia mahitaji yao.

4. Kuwatia moyo watumishi juu ya neno wanalohubiri na maombi wanayofanya kwa watu mbalimbali.
Katika Marko 16:20 imeandikwa hivi:

"Nao wale wakatoka, wakahubiri kotekote, Bwana akitenda kazi pamoja nao, na kulithibitisha lile neno kwa ishara zilizofuatana nalo"

Watumishi wa Mungu wanaposikia mambo ambayo Yesu anafanya wanaposema neno lake au wanapoomba kwa Jina lake - wanatiwa moyo ya kuendelea katika huduma hizo.

Alichosema Mfalme Daudi
Mfalme Daudi katika Zaburi alizoziandika unaona kabisa anavyosisitiza umuhimu wa kusifu na kutangaza habari za Mungu wetu na matendo yake katikati yetu.
Katika Zaburi 96:2,3 anasema, " Tangazeni wokovu wake siku kwa siku, (kila siku hubirini) habari za utukufu wake, ((( habari za maajabu yake". Anaendelea katika mistari ya 4 hadi 6 kutoa sababu anaposema:

"Kwa kuwa Bwana ni mkuu mwenye kusifiwa sana. Na wa kuhofiwa kuliko miungu yote. Maana miungu yote ya watu si kitu, lakini Bwana ndiye aliyezifanya mbingu. Heshima na adhama ziko mbele zake, nguvu na uzuri zimo katika patakatifu pake".

Katika Zaburi ya 44:1, Mfalme Daudi anaeleza jinsi walivyoelezwa na baba zao habari za matendo makuu ya Mungu wao. Katika Zaburi za 92 na 98 anahimiza watu kusifu kwa nyimbo matendo makuu ya Mungu! Katika Zaburi ya 119:95,99 anaeleza jinsi anavyozitafakari na kuzifikiria shuhuda za Mungu! Lazima ndani yake alijua wazo linalosema; "There is no God like our God of Israel!".
Na sisi Je!
Nasi tunasema, "There is no Jesus like our Jesus Christ!" Ndiyo maana tumeona tuwe na ukurasa huu unaoleza mambo ambayo Mungu anayafanya wakati huu katika huduma alizotupa kwa njia ya Mwana wake Yesu Kristo. Nia yetu si kujiinua sisi katika haya utakayokuwa unayosoma, bali kumwinua Yesu Kristo, ambaye peke yake ndiye anayestahili sifa na heshima zote! Maana ni Yeye ndiye ayafanyae yote haya kwa uwezo wa Roho wake Mtakatifu!
Sasa endelea kusoma shuhuda hizi - zingine ni barua tulizoandikiwa na zingine ni maelezo tuliyoyachukua moja kwa moja:
NIMEPONA TUMBO LA UZAZI
Mpendwa Mtumishi wa Mungu
Ndugu Christopher Mwakasege.

Nakusalimu katika Jina la Bwana.
Ni matumaini yangu kwamba umzima pamoja na familia yako na Bwana anakuwezesha katika wito aliokuitia. Bwana asifiwe sana. Mtu wa Mungu nimeshindwa kunyamaza kwa makuu Mungu alionitendea siku ile ya tarehe 8/8/1999 siku ambayo ilikuwa ni ya mwisho wa semina uliyofundisha pale Diamond Jubilee.

Nilikuwa na shida kubwa ya tumbo la uzazi karibu mwaka wa pili sasa, naumwa lakini navumilia nikijua kwamba ipo siku Mungu ataniponya tu. Nilijificha sana ili shida hii wengine wasiijue lakini mume wangu alijua na alinitia moyo sana akaniambia Mungu atakuponya siku isiyokuwa na jina. Namshangaa Mungu siku ile ya Jumapili ulivyosema kila mtu ashike mahali panapouma nilishika tumbo langu sehemu ya uzazi. Ukaomba na mimi nilikuwa naomba ulivyosema kwamba Mungu amekuponya vidonda na uvimbe kwenye tumbo la uzazi.

Mtumishi wa Mungu ni kwamba ile hali niliyokuwa nayo ya kutisha hata kukaa nilikuwa napata shida sana kwa jinsi ambavyo damu zilikuwa zinatoka lakini muujiza nilioupata ni kwamba damu zilikauka pale pale na ndipo nilijua na kukumbuka maneno mume wangu aliyokuwa ananifariji nayo kuwa siku isiyokuwa na jina Mungu atakuponya; kweli ni ajabu namshukuru sana Mungu kwa tendo hili kubwa kwangu. Mungu azidi kukubariki katika utumishi huu; na azidi kukutumia katika nyakati hizi za mwisho. Katika macho ya kibinadamu hunijui lakini macho ya kiroho unanijua hata na sura yangu maana Mungu alikuonyesha shida yangu.

(- toka Dar es Salaam)
NIMEPONA KUPITIA MAJARIDA YA MANA
Wapendwa katika Kristo Yesu
Baba C. Mwakasege na Mama D. Mwakasege.
Ninayo matumaini makubwa kwa upendo wake Mungu Baba kuwa Mungu anawatia nguvu, mu ngali bado wazima kimwili na kiroho.
Namshukuru Mungu yeye yule jana, leo na hata milele anayenitia nguvu kila iitwapo leo. Nilikuwa na jeraha moyoni, Mungu awabariki kwa kuniponya kupitia majarida ya MANA mliyonitumia. Na washukuru sana Mungu awasaidie kwani ALICHOANZISHA MUNGU shetani HAWEZI KUZUIA.
1. Naomba tuzidi kuombeana na Mungu awabariki kujitoa kwenu.
2. Naomba maelezo zaidi juu ya huduma yenu.
3. Nategemea majarida matoleo mengine toka kwenu

(- toka Tukuyu)
SHUKRANI YA PEKEE
Hii ni shukrani kwa Mungu kwa mambo makuu ambayo Mungu amenitendea.
1. Amemponya mtoto wangu aliyekuwa katika hali mbaya sana ya ugonjwa.
2. Terehe 20/02/2000 katika semina ya C. Mwakasege mtoto huyo aliokoka na kukabidhi maisha yake kwa Bwana Yesu.
Hivyo basi ninaomba shukrani hii itumike kama mchango katika huduma ya mikutano au semina hizo za Mwakasege ili wengine nao waje kwa Yesu. Ninamtolea Mungu shs. 20,000/=

(- toka Dar es salaam)
NIMEPONA KIFUA
Mpendwa C. Mwakasege, Bwana asifiwe.
Ninakusalimu kwa jina la Bwana Yesu. Mwaka jana (1999) nilikuandikia barua nikihitaji uniombee. Nilikuwa na maumivu kifuani ambayo hayakujulikana yanatokana na nini, ingawa nilipiga x-ray.
* Ninayo furaha kukushukuru kwa maombi yako kwani Bwana Yesu aliniponya.Roho wa Mungu alinionyesha katika ndoto kuwa unaniombea. Ninamtukuza na kumbariki Bwana!!
* Ikiwezekana ninaomba na mimi, nitumiwe gazeti (Jarida) la MANA ili tushirikiane baraka za Mungu.

(- toka Dar es Salaam)
KITABU CHA DAMU YA YESU KIMENISAIDIA
Mpendwa katika Bwana.
Tumsifu Yesu Kristo, Mimi nimeolewa ni mama wa watoto watano pia ni mkatoliki.
Nimepata mengi sana baada ya kusoma kitabu chako cha "Fahamu Uwezo wa Damu ya Yesu Kristo". Nimekubali kweli Mungu alikuwa na mpango nami kuweka hicho kitabu mikononi mwangu. Kwani mambo yote yaliyoandikwa nimeyaweka katika matendo na nimeona majibu, ya ukweli kabisa yaani HAI kabisa Jina la Bwana libarikiwe. Kabla ya kusoma kitabu hicho nilikuwa na shida nyingi mno kiroho pia kimwili.

Lakini Mungu ni wa ajabu sijui Ndugu nikueleza nini; kwenye barua siwezi ni mengi mno. Ninachosema tu ninamshukuruni sana Mungu Baba wa Mbinguni, ninaishukuru pia sana tu Damu ya Yesu Kristo kwa yote hayo niliyoyapata.
Uzima wa milele nimeuona katika damu ya Yesu, uzima, uponyaji, amani, upendo, utajiri na kufanikiwa na baraka zingine za Mungu.

Maisha ya ndoa nilikuwa ninayaona magumu sana!! Lakini sasa sivyo, kwenye ukurasa unapotaka kusafiri ufanye nini? Mungu amenitendea makuu pamoja na Damu ya Yesu.
Sasa ndugu ninachokuomba, tafadhali unitumie vijitabu vingine au makaratasi mengine ili niweze kuimarika zaidi katika Neno la Mungu, kwani mambo yote yatapita lakini Neno litasimama.

Pia katika sala zako uniombee ili nizidi kuimarika zaidi na zaidi.
Ninasubiri kwa hamu kuliko yule anayesubiri kufunga harusi. Nikitumaini Bwana atakugusa kwa njia ya pekee uweze kunitumia hivyo vijitabu vya Neno la Mungu.

(- toka Morogoro)
NIMEPONA TUMBO LA UZAZI
Mtumishi wa Mungu.
Bwana asifiwe.

Ninakuandikia, kumrudishia Mungu utukufu kwa matendo makuu aliyonitendea. Siku ya tarehe 6/8/1999 nilipokea uponyaji.

Nilikuwa ninasumbuliwa na tumbo la uzazi Mwezi Machi/1999 nilipata tatizo la kutoka damu muda mrefu. Nilikwenda hospitali nikasafishwa - lakini ziliendelea mwezi mzima. Mwezi April na May nilipata damu kwa matatizo. Mwezi wa sita tatizo liliongezeka, damu zilikatalia tumboni. Nilipata taabu sana. Nilikuwa likizo wakati huo. Nikiwa na mama yangu - siku moja usiku niliona kifo kiko mbele yangu. Mama ameokoka katika huduma yako pale Iringa.

Alisogea kitandani akaniuliza vipi? Kwa kutaka nisimfadhaishe, nilimwambia niombee, akaomba, nikalala asubuhi yake nilianza kupata nafuu tangu tarehe 1 / 7 zilikoma 14/7. Tarehe 2/8 tatizo lilianza tena. Tarehe 6/8 wakati maombi yanaendelea wakati wa semina yako, Diamond Jubilee, nikiwa pale mbele, nilipokea uponyaji, damu ziliacha kububujika palepale. Mpaka dakika hii naandika - nimepona kabisa. Asante Yesu.

(- toka Dar es Salaam)
NINA NENA KWA LUGHA
Dhumuni la barua hii ni kushukuru kwa nakala ya kitabu cha Hongera kwa Kuokoka nasema ahsante Mungu akubariki. Nilifurahishwa sana na semina ambayo ilifanyika kanisani ARUSHA mjini kati.
Nilifurahi kwa sababu nilipata mambo mengi nilijiona nilikua niko nyuma sana lakini sasa naona Mungu ananisaidia na furaha yangu kubwa zaidi ni kwamba nilikua sina Roho Mtakatifu lakini semina hiyo nilifaidi nilikua sijawahi kunena kwa lugha lakini nilifurahi sana sasa nina Roho Mtakatifu ninanena kwa lugha, nina furaha isiyokifani.(kupitia kwa mwalimu mwakasege.org)

No comments:

Post a Comment

mwakasege A moment of worship

ushuhuda