KWA NINI BWANA YESU ALITUOMBEA
UMOJA?
Wiki ya Kwanza
UTANGULIZI
Mungu tunayemwamini katika Yesu Kristo, ni Mungu wa mipango na makusudi
kamili. Tangu vizazi na vizazi tabia hii ya Baba yetu, imejidhihirisha
wazi.
Baba yetu huyu, ambaye pia, ni Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, hawezi
kufanya kitu au kusema kitu, bila ya kuwa na sababu.
Mungu aliumba dunia hii, kwa kusudi kamili, ili ikaliwe na watu isiwe
tupu.
Mungu aliumba jua, mwezi, sayari na nyota mbali mbali, kwa makusudi
kamili, ili viwe ndiyo dalili za majira na siku na miaka na tena iwe
ndiyo mianga katika anga la mbingu itie nuru juu ya nchi.
Mungu alimtokea Musa katika kijiti kilichokuwa kikiwaka moto, kwa kusudi
kamili, ili apate kuwatoa watu wake, wana wa Israeli kutoka Misri.
Mungu alimtoa Mwana wake wa pekee Yesu Kristo, kwa kusudi kamili, ili
kila amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.
Mungu
alimwaga Roho wake Mtakatifu juu ya watu wake, kwa kusudi kamili, ili
wapate nguvu ya kuwawezesha kuwa mashahidi wa Kristo katika ulimwengu
mzima.
Ni kweli kabisa ya kwamba, Mungu tunayemwamini katika Yesu Kristo, ni
Mungu wa mipango na makusudi kamili. Hafanyi kitu bila ya kuwa na sababu
nacho.
Kwa
hiyo alipokuwa akisema na watumishi wake, alikuwa na kusudi na ujumbe
kamili kwa ajili ya watu wake.
Na
aliponiita kwenye utumishi wake alikuwa na mipango na makusudi kamili
kwa ajili ya watu wake. Kwa hiyo niliposikia sauti yake ndani ya roho
yangu nilipokuwa kwenye mkutano wa ‘Easter Crusade’, Tukuyu, Mbeya
Aprili 1987, nilijua hakika ya kuwa kuna jambo la muhimu.
Nilisikia
sauti ya Bwana ndani ya roho yangu ikisema; “NATAKA KUSEMA NA WATU
WANGU”.
Si
kwamba nilisikia sauti kama ya mtu akiongea; hapana; bali kwa uwezo wa
Roho wake Mtakatifu, nilisikia sauti hiyo ndani ya roho yangu. Na
nilijua hakika ya kuwa hiyo ni sauti ya Bwana wangu na Mwokozi wangu.
Hata Yeye alisema kuwa ndiye pekee aliye mchungaji mwema, walio wake
anawajua, na wao wanamjua, na sauti yake wanaijua (Yohana 10:1-6).
Mkutano
huo wa kiroho ulikuwa umejumuisha watu wa Mikoa mbali mbali na pia watu
wa madhehebu mbali mbali. Na Bwana aliposema nami kwamba anataka kusema
na watu wake ilikuwa ni mchana wa siku ya pili ya mkutano.
Kwa
hiyo baada ya kusikia hivyo, nilitafuta mahali pa faragha katika chumba
kimoja; nikapiga magoti, na nikawa tayari kusikia lile ambalo Bwana
alikuwa anataka lisikike kwa watu wake.
Maneno
aliyoniambia yalihusu juu ya UMOJA WA WATU WAKE. Na waliokuwapo kwenye
mkutano huo walipata nafasi ya kusikia kwa muhtasari tu, juu ya Umoja wa
watu wa Mungu.
Maneno
hayo ya Bwana juu ya umoja wetu ni muhimu sana. Na kwa ajili hiyo,
Roho wa Bwana ameniongoza kuyaandika kwa undani zaidi, ili watu wengi
waweze kuyapata na kuyafanyia kazi.
Jambo
ambalo Bwana analiona katikati yetu, katikati ya wakristo, ni kukosa
Umoja wa kweli. Na jambo hili linamhuzunisha sana Mungu. Hii ni kwa
sababu watu wake ndiyo mwili wake (1Wakorintho 12:27). Kwa hiyo kukiwa
na nyufa katika uhusiano wa mkristo na mkristo mwingine, maana yake
mwili wake umepata nyufa.
Kusudi
lake kubwa la kutulinda, kututunza, kutulisha, kututakasa na kutuongoza
ni ili atulete mbele za Baba yetu aliye mbinguni, bila waa na wala
kunyanzi.
Lakini,
hali inayoonekana sasa ni ya kusikitisha. ‘Fellowships’ nyingi
hazina umoja na zimetawaliwa na mafarakano. Viongozi wa Kanisa nao pia
hawana umoja kila mmoja anafanya mambo yake mwenyewe, ambayo anayaona ni
bora kuliko ya mwenzake. Vikundi vingi vya huduma za kikristo havina
umoja wa kweli.
Yesu
Kristo alituombea umoja. Je! Maombi yake yamejibiwa au bado? Na alikuwa
na sababu gani alipokuwa anatuombea? Je! Yesu Kristo alikuwa na mpango
wowote aliouandaa juu ya umoja wa mwili wake, ambalo ni Kanisa?
Ni
nini chanzo cha mafarakano na kukosa umoja katikati ya watu wa Mungu?
Tufanye nini ili tupate kusimama katika umoja wa kweli?
Maswali
hayo na mengine yanajibiwa katika somo hili.
Sasa, ngoja niseme jambo moja muhimu:
Mungu
huyu tunayemtumika ni Mungu aliye na kusudi kamili, katika kila jambo
analolifanya na kulisema. Na kwa mtazamo huu, nakuambia hivi, Mungu
ameweka maandiko ya somo hili mikononi mwako kwa kusudi kamili, kwa
ajili ya utukufu wa Jina lake Takatifu.
Kwanza:
Kwa sababu anakupenda upeo, hapendi upotee.
Pili:
Kwa sababu wewe ni kiungo cha mwili wake, ambao ndilo Kanisa
Tatu:
Kwa sababu anataka uhusike moja kwa moja katika kushirikiana na Roho
wake Mtakatifu, ili kuwashirikisha wengine ujumbe huu.
Ni
maombi yangu kwa Mungu katika Jina la Yesu Kristo aliye hai, ya kuwa
Roho wake akutie nuru katika utu wako wa ndani upate kuyaelewa yote na
kuyafanyia kazi ipasavyo. Na ukiishayasoma uwashirikishe wengine bila
kuyapindua pindua.
Hizi
ni siku za mwisho, na tunatakiwa tuwe waangalifu katika yote
tunayoyasikia au kuyasoma. Tunatakiwa tuyachambue, na kuyapima, halafu
tuyachukue yaliyo mema yanayotujenga pamoja na siyo kutubomoa.
Kwa
hiyo nakushauri, katika Jina la Yesu Kristo, ya kwamba unapoyasoma
yaliyomo humu, uwe na BIBLIA yako karibu upate kuifuatilia mistari yote
niliyoinukulu. Bwana na akuwezeshe kuyatafakari na kuyafanyia kazi ili
wote tuwe na Umoja kama Baba na Kristo walivyo umoja.
Sifa
na Utukufu na uweza, na nguvu vina Mungu wetu katika Kristo Yesu, milele
na milele – Amina.
YESU
KRISTO ALIOMBA UMOJA KWA AJILI YA NANI?
Neno Umoja maana yake nini?
Yesu
Kristo alipokuwa anaomba juu ya Umoja kama ilivyoandikwa katika kitabu
cha Yohana sura ya kumi na Saba, alilitumia neno Umoja mara tano.
Neno
Umoja linaweza kuwa na maana mbali mbali, kutokana hasa na mtu
anayelitumia, mahali anapolitumia na kwa ajili ya kitu gani.
Neno
Umoja likitumika kwa ajili ya watu lina maana ya patana, afikiana,
elewana na lingana, katika roho, na nia, mawazo, maneno na matendo.
Yesu
Kristo alipokuwa akitumia neno Umoja, alikuwa anamaanisha hao
anaowaombea wapatane, waafikiane, waelewane, na walingane katika roho
zao, nia zao, mawazo yao, maneno na matendo yao.
Sasa,
hili si jambo dogo!
Yesu
Kristo alipokuwa hapa duniani, akiwa amevaa mwili wa kibinadamu; kabla
ya kufa na kufufuka; aliomba maombi ya namna nyingi.
Na
mojawapo ya maombi yake kwa Baba Mungu, yalikuwa juu ya Umoja wetu.
“Wala
si hao tu ninaowaombea; lakini na wale watakaoniamini kwa sababu ya neno
lao. Wote wawe na Umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani
yako; hao nao wawe ndani yetu; ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba
wewe ndiwe uliyenituma. Nami utukufu ule ulionipa nimewapa wao; ili wawe
na umoja kama sisi tulivyo umoja. Mimi ndani yao; nawe ndani yangu, ili
wawe wamekamilika katika umoja; ili ulimwengu ujue ya kuwa ndiwe
uliyenituma, ukawapenda wao kama ulivyonipenda mimi
(Yohana 17:20 – 23).